MAKALA: Tumia kidogo ulichonacho kuelekea kwenye mafanikio yako



Habari za leo ndugu msomaji wa makala za Rise Africa. Ni wakati mwingine tena, kujifunza pamoja kuhusu mambo mbalimbali ili kufikia mafanikio tuliyojiwekea kila siku.
Watu wengi duniani wanahitaji maisha mazuri, kuwa na fedha za kutosha zitakazogharamia chakula kizuri, nyumba nzuri au gari zuri. Kwa ujumla, wanahitaji kuwa matajiri.
Licha ya kuyatamani maisha hayo, tatizo ni njia ya kuwafikisha kwenye maisha hayo wanayoyaota kila siku. Leo, nitawafumbua macho wasomaji wa makala hizi kwa kuwawezesha kufahamu thamani na nguvu ya ulichonacho kupata unachokitaka.
Kipo kitabu cha Siri ya Watu wenye Furaha kinachoelezakuhusu mtu kutambua thamani yake na kutokata tamaa, ili kuyafikia mafanikio yake. Kwamba kila binadamu ni zaidi ya akaunti ya benki, ni zaidi ya akiba anayojiwekea benki au kwenye kibubu.
Binadamu ni wa thamani zaidi. Alichonacho ndani yake, kama ataamua kukitumia vizuri na kwa ukamilifu, ni kikubwa mno na kinaweza kumpatia utajiri, ufahari na umaarufu katika jamii yake, taifa lake na duniani.
Kitu cha muhimu kutambua ni kwamba hakuna mwanadamu asiyekuwa na kitu ndani yake. Lazima ana kipaji fulani ndani yake. Kinaweza kuwa cha uimbaji, uchoraji, ufundishaji, uchekeshaji, ukimbiaji, urukaji, uogeleaji, ubunifu wa mavazi, teknolojia au chochote kingine.
Kila binadamu ana kimojawapo kati ya vipaji hivyo na vingine ambavyo havikutajwa hapo juu ambacho akikitumia vizuri na kwa ukamilifu, kinaweza kumpatia utajiri na mambo mengi mazuri ambayo aliyoyatamani kuwa nayo katika maisha yake.
Unaweza kuanza kutumia kipaji chako bila kuwa na chochote kwa maana ya fedha kama mtaji. Kilicho muhimu kwako ni kugundua kitu cha thamani kilichomo ndani yako na kuamua kukitumia mara moja. Kuna watu wengi duniani wametajirika kutokana na vipaji walivyonavyo. Wengi wao hawakuwa na kitu bali thamani yao au talanta zao ambazo walizitumia vizuri na kufanikiwa kimaisha.
Mungu amempa kila mtu kitu cha thamani ndani yake. Hakuna mtu ambaye hana kitu. Tatizo ni kwamba wengi hawajijui kama wana kitu hicho chenye thamani kubwa.
Hakuna haja ya mtu kufanya vitu vya fedheha na aibu kama vile kupiga picha za utupu ili kupata fedha, bali kutumia kitu cha thamani ulichonacho kupata umaarufu wa thamani badala ya umaarufu wa fedheha. Umaarufu wa mtu unaotokana na kipaji unadumu duniani kwa miaka mingi hata vizazi vijavyo vitajifunza kutokana na umaarufu huo.
Fedha au umaarufu unaotokana na vipaji, uwezo, nguvu, ubunifu na kadhalika, huwa ni wa kudumu, haufutiki duniani. Huu ni umaarufu tofauti na wa kutengeneza skendo za ngono na mambo mengine ya aibu na fedheha yasiyompendeza Mungu.
Ni umaarufu utokanao na uimbaji, uandishi wa vitabu, ugunduzi wa magari, ndege au meli pamoja na teknolojia mbalimbali. Waliowahi kufanya hivyo wameacha majina yao duniani na kamwe hayatasahaulika.
Hawatasahaulika kwa sababu walifanya mambo ambayo yanaendelea kuishi ulimwenguni hapa hata kama wao wametangulia mbele za haki. Mchango wao mwema umebaki kuwa urithi kwa vizazi vilivyofuata.
Ni wakati wetu, wewe na mimi kujiuliza tulichokifanya mpaka sasa hapa duniani au tulivyotumia uwezo wetu wa ndani kulingana na kipaji ambacho kila mmoja amejaliwa.
Matumizi sahihi ya kipaji au talanta uliyobarikiwa ndiyo yataamua utakachokiacha duniani baada ya kifo chako. Wapo wanaokubali kufa na kusahaulika kirahisi kwa bila kuacha jambo lolote walilolifanya, ambalo litaendelea kuishi na kugusa maisha ya watu wengine wanaowaacha na watakaokuja duniani.
Kila mmoja anapaswa kufahamu kwamba inawezekana kufanya mambo makubwa hata kuliko ya waliotutangulia ambao kwa miaka mingi tangu waondoke duniani, majina yao bado yanaishi.
Ni ukweli ulio dhahiri kwamba kila mmoja anacho kitu kikubwa ndani yake, yeye binafsi ambacho wengine hawana na dunia nzima hakuna mwenye nacho isipokuwa yeye tu.
Ipo falsafa moja moja muhimu. Mafanikio huja baada ya kutatua tatizo la mtu mwingine. Kipaji ulichonacho unapaswa ukitumia kuwaridhisha wengine na kwa kufanya hivyo watakuwa tayari kulipia huduma yako.
Hapo ndipo mafanikio yako yatakapoanza kuonekana. Uchumi wako utaanza kukua. Kama ni muimbaji, utakapofanya matamasha na kuwaburudisha watu kiingilio chao kitakuwa kipato chako.
Hata wachekeshaji, utakapofanikiwa kuwachekesha walionuna, hawatasita kukulipa. Anza sasa kukitumia kipaji chako kubadilisha maisha ya jamii inayokuzunguka, familia yako, taifa lako na dunia kwa ujumla. Kubwa zaidi ni maisha yako binafsi.
Hajawahi kutokea mtu yeyote aliyetumia vyema kipaji chake na asifanikiwe. Wote unaowafahamu wamefanya kitu tofauti na wengine. Waorodheshe huku ukijikumbusha kuwa nawe unachoweza zaidi ya wengine.
Kama kuna maswali karibuni tuyajadili kwa pamoja.
Asante sana.

Related Posts

Latest