MAKALA: Busara, hekima vina mchango kwenye mafanikio yako kiuchumi

Kwenye kila kinachofanywa, kuna uhusiano kati ya hekima na busara za mtu na mafanikio yake kimaendeleo ya kiuchumi.
Kwa hekima mtu hupanga mikakati yake na kwa busara alizojaaliwa huomba ushauri na kutafuta taarifa muhimu kabla ya kuanza kutekeleza anachokiamini. Kwa utaratibu huu, uwezekano wa kupata mafanikio ni mkubwa.
Hili ni kwa masuala yoyote ambayo mhusika anakusudia kuyatekeleza. Iwe kazini, kwenye biashara zake au kwenye masuala yanayohusu jamii inayomzunguka. mipango sahihi na ushawishi uliopangiliwa hufanikisha jambo hata liwe gumu kiasi gani.
Ili kuwa mtu mwenye hekima huna budi kuijenga mienendo anayotakiwa kuwa nayo mtu mwenye hekima upeo mwafaka, maadili na kupanuka kwa akili. Hivi vyote viwe amali iliyo mwilini na maishani mwako.
Anza kujifunza kuwa mtu mwenye hekima na hatimaye zitumie hekima hizo katika maisha yako ya kila siku.
Pili, ushauri nasaha. Kuwa mtu mwenye hekima ni mazoezi ya kujiendeleza ndani kwa ndani; ndani ya moyo wako! Na kwa kweli kuna shughuli ambazo ukizifanya zinakupeleka ilikojificha hekima.
Mafunzo kutoka kwa wataalamu na washauri nasaha yatakufikisha mahali pa kuanzia kuelekea kwenye hekima yenyewe.
Ukishafika hapo utaanza kupanda ngazi kuelekea juu zaidi. Hatua hii tunaweza kuiita hatua ya mtu mkomavu. Mtu aliye katika hatua hii amefikia kiasi cha kuweza kudhibiti hisia zake.
Anakuwa anaweza kuyajua mateso, kwa kiasi chake, ayapatayo mwenzie kama yale anayoyapata yeye.
Kuna aina nyingi za ushauri nasaha; namna ya kuyatawala maisha yako, kuondokana na hofu, namna ya kuweza kuitawala hasira, kuachana na ‘uteja’ wa jambo fulani na mambo mengine mengi kama hayo.
Tatu, kusoma kunaweza kutupeleka ilipo hekima. Kusoma mambo yanayohusu maendeleo ya ndani mwako kwaweza kuwa msaada mkubwa kwako kama unataka kuwa mtu mwenye hekima. Anza kujisomea mambo yatakayopanua upeo wako.
Masomo hayo yatakuongoza kufanya mazoezi mwenyewe ukiwa peke yako. Mazoezi ya kutuliza akili, kujijua undani wako au ya kupaisha uwezo wako kiasi cha kufanikisha mipango na mikakati uliyojiwekea maishani.
Kujisomea siyo kitu mbadala cha mazoezi yenyewe isipopkuwa kwaweza kushawishi kuanza kuyafanya mazoezi tuliyoyasoma.
Riwaya, tamthilia na vitabu vinavyoelezea maisha ya watu maarufu ni rasilimali muhimu ziwezazo kukuelimisha kuhusu hekima kwa vitendo. Kwa kuwa vitabu hivi vinakupa mifano halisi ya tabia za hekima na tabia zisizo za hekima; utatuzi wa mambo ya kimaisha bila kutumia nguvu kubwa.
Vitabu vinavyoelezea maisha ya watu maarufu vinaweza kuwa vya msaada mkubwa. Husaidia kuelewa namna tabia za watu hawa zinavyotofautiana na watu wa kawaida na maadili yanayoongoza maisha yao au upeo wa maisha wanaoutumia.
Kama tunataka kuwa katika kundi la watu wenye nia ya kuibadilisha dunia, hatuna budi kuchagua rasilimali zitakazotusaidia kufikia mabadiliko tuyatakayo. Moja ya raslimali hizo ni maarifa mapya yanayohusu sayansi, mabadiliko ya ulimwengu au afya pia.
Rasilimali nyingine ni kujifunza zaidi kuhusu utamaduni, mifumo ya uchumi na undani kuhusu ardhi. Rasilimali nyingine ya jumla ni kuelewa kuhusu maadili na mbinu za kubadili upeo wa kimaadili.
Inaweza kujuisha ujuzi wa kutatua migogoro, uwezo wa kuongea kwa mvuto na kujua mambo yote yanayotokea kwa lengo la kuibadili dunia.
Nne, uzoefu wa maisha. Kama tumejitolea kujifunza, maisha yenyewe ni mwalimu! Kwa kuwa na uzoefu wa mambo mengi tunakuwa tumetanuka kiupeo. Siyo tu tunatakiwa kuyagawa maisha yetu ili tuwe na uzoefu wa aina nyingi, bali kufungua akili zetu ili tuweze kufaidi uzoefu uliotamalaki dunia.
Katika kukuza uzoefu wako kwenye masuala tofauti ya maisha, ni busara kujuana na watu wenye ujuzi tofauti na wako kwa kufahamiana na watu wenye mtazamo tofauti na wako pia.
Juana na watu wenye maadili tofauati na yako bila kuwaacha wanaofanyakazi tofauti na yako na usiache kushiriki michezo na matukio mbalimbali yanayofanyika kwenye jamii inayokuzunguka. Mambo haya yote uongeza upeo katika maisha yetu na kutuongoza kwenye njia ya kuelekea kwenye hekima.
Tano, ushauriwa kujifunza kutoka kwa watu wenye hekima. Kaa karibu na watu ambao ungependa wawe mashujaa wako. Ni jambo jema kukaa na watu ambao ni waumini wa maadili unayoyataka. Ni msaada kwako. Makundi yanayojishughulisha na kuwaamsha watu kujitambua na kukua kiakili na kiroho yanasaidia sana.
Kuna mijadala ya kukuza upeo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii. Jaribu kujifunza toka kwenye vikundi hivyo. Baadhi ya vikundi hivi hujishughulisha na kukua kisaikolojia na kiroho. Vingine kujishughulisha na mambo ya kijamii. Fanya utafiti ukiona kundi linaloendana na wewe ujiunge.
Sita, chunguza tabia zako na za wengine. Watu wote wanaotuzunguka wapo katika harakati za kutaka kuishi maisha bora zaidi ya wengine wanaofanya harakati hizo kwa kutumia ujuzi kwa mafanikio.
Tunaweza kutambua mikakati na tabia nzuri na mbaya kwa kujifunza tabia, kwa kuanza na zetu na kujijua tupo katika kiwango gani cha maadili. Kwa kufanya hivi tunaweza kujua kiundani zaidi kuhusu maadili.

Related Posts